Wabunge Kenya kuamua kuhusu uwakilishi wa jinsia


Wabunge nchini Kenya wanatarajiwa kupiga kura, kwa mara nyingine, ya kupitisha ama kupinga mswada wa sheria kuhusu usawa wa jinsia katika nyadhifa za uteuzi na siasa.
Kwa mujibu wa Katiba ya Kenya, nyadhifa zote za uteuzi na uchaguzi katika afisi za umma hazifai kuchukuliwa na zaidi ya theluthi mbili ya jinsia moja, iwe wanawake ama wanaume.
Wiki iliyopita mswada huo ulifeli ambapo ni wabunge 195 pekee waliouunga mkono, 28 wakaupinga, wawili wakakosa kutangaza msimamo wao huku 24 wakikataa kupiga kura.
"Tuna matumaini kuwa mswada huu utaptishwa hivi leo, tumekuwa tukizungumza na wenzetu wanaume, na kuwarai kutuunga mkono, na tuna matumaini,” anasema mbunge Cecily Mbarire ambaye ni mwenyekiti wa muungano wa wabunge wanawake nchini Kenya
Wabunge 233 wanahitajika kupitisha mswada huo muhimu.
Hata hivyo kura ya kupitisha mswada huu inajiri siku ya mwisho kabla ya wabunge kwenda likizoni, na kwa kawaida kikao kama hicho huhudhuriwa na wabunge wachache.
Wabunge wanatarajiwa kwenda likizo ya mwezi mmoja baada ya kikao cha leo alasiri.
Rais Uhuru Kenyatta, ambaye ni kiongozi wa muungano wa Jubilee, ulio na wanachama wengi bungeni, amewaomba wabunge kupitisha mswada huo.
OdingaImage copyrightAFP
Image captionBw Odinga amesema atahudhuria kikao cha leo cha Bunge
Kiongozi wa upinzani Raila Odinga ametoa ombi sawa na hilo kwa wabunge wa muungano wake wa CORD.
Katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2013, wanawake hawakuchaguliwa katika nyadhifa za ugavana na useneta.
Kati ya wabunge 290 waliochaguliwa na wananchi mwaka 2013, asilimia 5.5 pekee ya wanawake ndio waliochaguliwa.
Kati ya wawakilishi wa wodi 1450, ni wanawake 88 pekee waliochaguliwa.
Bunge la kenya linajumuisha wabunge 290 waliochaguliwa na wananchi, wabunge 47 wanawake waliochaguliwa na wananchi kuwakilisha kaunti 47, na wabunge 12 maalum walioteuliwa na vyama vya kisiasa na spika wa bunge.

No comments:

Post a Comment

PERUZI24HOURS Designed by Templateism Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.