Latest News

SIMBA KUNOGA KWA MABALIKO


HATUA ya kwanza ya safari ya kuelekea kwenye mabadiliko kwa Simba inaanza leo, baada ya Kamati ya Utendaji ya timu hiyo kupokea maoni ya wanachama wake.
Simba ipo kwenye mchakato wa kuwa Kampuni ambapo mwanachama wa klabu hiyo na mfanyabiashara maarufu Mohamed Dewji ‘Mo’ yupo tayari kununua hisa asilimia 51 kwa Sh bilioni 20.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa Simba, Patrick Kahemele alisema kamati ya utendaji leo inatarajiwa kupokea maoni ya kamati maalumu iliyoundwa kukusanya maoni ya wanachama juu ya safari ya mabadiliko.
“Rais Aveva (Evans) na kamati yake ya Utendaji waliunda kamati ya kuratibu maoni ya wanachama juu ya mabadiliko ambayo klabu inataka kuyafikia hivyo kesho (leo) kamati itayawasilisha,” alisema.
Wanachama wa Simba waliridhia kwenda kwenye mabadiliko mwishoni mwa wiki iliyopita walipokutana kwenye mkutano mkuu uliofanyika Dar es Salaam.
“Lengo letu ni kwenda kwenye mabadiliko, ya aina gani? Tunasubiri maoni ya wanachama wetu kisha majibu yatatolewa, lakini ni mchakato unaohitaji uvumilivu kidogo maana kuna vitu vingi vya kuzingatia,” alisema Kahemele.
Awali Mo aliahidi kuisaidia Simba kwenye usajili endapo itakubali kufanya mabadiliko ya kutoka klabu kumilikiwa na wanachama mpaka kuwa ya wanahisa, jambo ambalo juzi alilitimiza kwa kuipa Simba mfano ya hundi ya Sh milioni 100.
“Mimi nimeamua kusaidia usajili wa Simba na leo (juzi) nimewapatia Sh milioni 100 naamini zitasaidia,” alisema.
Akizungumzia fedha hizo, rais Aveva alisema: “Fedha hizi zitasaidia kufanya usajili wa M-Ivory Coast, tulihitaji Sh milioni 420 ili kukamilisha sehemu ya usajili iliyobaki hivyo bado tunahitaji Sh milioni 320 kukamilisha usajili,” alisema ingawa hakusema bajeti nzima ya usajili ya klabu hiyo ni kiasi gani.

No comments:

Post a Comment

PERUZI24HOURS Designed by Templateism.com Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.