Latest News

MADEAMA MSHAMBULIAJI AMKOSHA KOCHA AZAM


KOCHA Mkuu wa Azam FC, Zeben Hernandez amemmwagia sifa mshambuliaji mpya wa timu hiyo raia wa Ghana, Enoch Atta Agyei kutokana na uwezo mkubwa aliouonesha siku ya kwanza alipojiunga kwenye mazoezi ya timu hiyo.
Agyei ametua Azam FC kwa mkataba wa miaka miwili akitokea Medeama ya Ghana na juzi alianza rasmi mazoezi na timu hiyo huku akikabidhiwa jezi namba 10 iliyokuwa ikivaliwa na M-Ivory Coast, Kipre Tchetche.
Akizungumza na gazeti hili jana, Hernandez alisema Agyei ameonesha uwezo mkubwa katika mazoezi yake ya siku ya kwanza na amemtabiria kuipa mafanikio makubwa timu hiyo kama atapata ushirikiano wa karibu kutoka kwa wachezaji wenzake.
“Ni mchezaji mwenye kipaji na ndiyo sababu nikautaka uongozi uhakikishe unamsajili baada ya kumuona wakati timu yake ikicheza na Yanga kwenye mchezo wa hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika, na kwa uwezo aliokuwa nao nadhani mashabiki watamsahau Tchetche,” alisema Hernandez.
Kocha huyo alisema kutua kwa mchezaji huyo kwenye kikosi chake kunamfanya akamilishe hesabu zake za kuimarisha safu ya ushambuliaji na sasa anaangalia zaidi kwenye safu ya kiungo na ulinzi ambayo bado kuna wachezaji anawaangalia kabla ya kuwapitisha ili waweze kuwasajili kwa ajili ya msimu ujao.
Alisema anataka kuunda kikosi imara kitakachoendana na uwekezaji uliofanywa na uongozi wa timu hiyo na kuwa kubwa Afrika na hilo linawezekana kwa sababu tayari wana nyota wengi kutoka mataifa mbalimbali ambao wanawafanyia majaribio na wameonesha viwango vya juu.
Azam hivi karibuni ilipiga kambi ya wiki moja Zanzibar na kucheza mechi mbili za kirafiki na kabla ya kucheza na Yanga Agosti 17, kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii inatarajiwa kucheza mechi mbili za kirafiki na timu za Majeshi za JKT Ruvu na Ruvu Shooting kwenye uwanja wake wa nyumbani Chamazi Complex.

No comments:

Post a Comment

PERUZI24HOURS Designed by Templateism.com Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.