Latest News

DC-Wanafunzi 16 wanapata mimba kila siku


MKUU wa Wilaya ya Kahama, Fadhili Nkurlu amesema takwimu za kitaifa zinaonesha kuwa kila siku wanafunzi 16 wanapata ujauzito mkoani Shinyanga hivyo  kusababisha washindwe kutimiza ndoto zao.
Ameyasema hayo jana katika Mkutano Mkuu wa Istiqaama Muslimu Community of Tanzania (IMCOT) uliojumuisha wajumbe 20 wa Taasisi hiyo kutoka Tanzania Bara na Visiwani, lengo likiwa kujadili malengo ya taasisi hiyo katika masuala ya elimu na afya.
Alisema katika baadhi ya vijiji hapa wilayani hakuna shule za msingi wala sekondari, hali ambayo inasababisha watoto wengi kutoenda shuleni.
Takwimu hizo za watoto kupata ujauzito, itazidi kuongezaka kama serikali na taasisi za kidini, zitashindwa kushirikiana.
Nkurlu alisema, serikali inatambua uwepo wa taasisi za kidini na ushirikiano wao katika jamii na kuwataka kushirikiana pamoja katika kutokomeza mimba za utotoni kwa kutoa elimu kwa jamii ili Watanzania wawe na hofu na Mungu kutokana na ujumbe utakaotolewa.
Mwenyekiti wa Taifa wa Taasisi hiyo, Seifu Ally Seifu alisema, lengo la taasisi hiyo ni kuwa karibu na waamuzi pamoja na jamii katika kutekeleza masuala ya afya na elimu hapa nchini.
Alisema tangu kuanzishwa kwake 1995, imejenga shule za msingi na sekondari 14, lengo likiwa kutoa elimu kwa jamii na kupunguza wimba la vijana kuwapo mitaani na kupatiwa elimu kutoka katika shule hizo.
Seifu alisema jukumu la kujenga shule pamoja na kutoa elimu kwa jamii sio la serikali pekee, bali ni la jamii nzima na kuongeza kuwa, kama jamii itaiachia serikali pekee, ongezeko la watoto wasio na elimu, litakuwa kubwa.
Shehe wa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Ismail Makusanya alisema utawala ulipo lazima ukubali kupata fikra kutoka kwa watu wengine ili kujua wapi walipo na wapi wanakwenda ili kujenga utawala bora.

No comments:

Post a Comment

PERUZI24HOURS Designed by Templateism.com Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.