KIKOSI cha watu 30 cha Yanga kimetua salama katika mji wa Sekondi - Takoradi, Ghana kikiwa na siri nzito juu ya mikakati ya kuwadhibiti wapinzani wao Medeama ya Ghana katika mchezo ujao wa Kombe la Shirikisho Afrika utakaochezwa keshokutwa.
Yanga itarudiana na Medeama kwenye Uwanja wa Sekondi-Takoradi ikiwa ni kilometa 213 kutoka Accra katika mchezo wa raundi ya pili hatua ya makundi, baada ya ule wa kwanza uliochezwa Dar es Salaam wiki iliyopita kutoka sare ya bao 1-1.
Akizungumza na gazeti hili jana kwa njia ya mtandao wa kijamii, Meneja wa Yanga Hafidh Salehe alisema walifika Takoradi juzi usiku wa saa moja ya kule, ambapo ni karibu saa nne kwa muda wa Afrika Mashariki.
Kwa upande wa Kocha Mkuu wa Yanga, Hans Pluijm alisema wangeanza mazoezi jana mchana kwa ajili ya kuzoea hali ya hewa ya kule. Alisema lengo la kufanya mazoezi mchana ni kwa sababu mechi yao itachezwa saa tisa kamili jioni kwa muda wa kule wakati Tanzania itakuwa ni kuanzia saa 12:00 jioni.
Pluijm alisema aina ya uchezaji na mfumo watakaoutumia ni siri yao kubwa kwani hawataki kuweka wazi kwani maadui zao wanaweza kuinyaka. Hata hivyo, kocha hakuweka wazi matatizo ya mchezaji huyo.
Kocha huyo aliyeipa timu hiyo mafanikio kwa kipindi cha miaka miwili, alisema ushindi katika mchezo utaamuliwa na wachezaji iwapo watacheza kwa moyo wa kujituma na kujitolea.
Yanga imefanya vibaya katika michezo mitatu ya raundi ya kwanza baada ya kufungwa dhidi ya TP Mazembe bao 1-0, dhidi ya Mo Bejaia bao 1-0 na kutoka sare mchezo wa mwisho dhidi ya Medeama bao 1-1. Kimsimamo Yanga inashika mkia katika Kundi A na inahitaji ushindi Jumatano ili kurejesha matumaini ya kufanya vizuri katika kundi lake hilo.
No comments:
Post a Comment