KOCHA Mkuu wa Yanga, Hans-van-der-Pluijm amesema mtihani mkubwa unaomkabili kwenye ligi ya msimu huu ni kusajili kiungo mkabaji kutoka nje ya Tanzania ili kufanya kazi moja ya kutibua mashambulizi ya timu pinzani.
Yanga imekuwa na mwenendo mbaya kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika hatua ya makundi na tatizo kubwa linaloisumbua timu hiyo Pluijm amesema ni ulinzi dhaifu kuanzia kwenye eneo la namba sita.
Akizungumza na gazeti hili jana, Pluijm alisema ameamua kumtafuta mchezaji huyo kutoka nje ya nchi kwa sababu Tanzania haina mchezaji wa aina hiyo na hata kama yupo atakuwa na mapungufu mengi ikiwemo kukosa nguvu za kupambana kwa ajili ya kuwalinda mabeki wake.
“Viungo tuliokuwa nao wanacheza vizuri lakini kuna sifa muhimu ambazo wanazikosa na ndio maana timu yetu imekuwa ikiruhusu mabao katika mechi zote tulizocheza za hatua ya makundi sasa nataka kulimaliza hilo tatizo kabla ya msimu mpya wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara kuanza,” alisema Pluijm.
Kocha huyo raia wa Uholanzi, alisema sifa za mchezaji anayemhitaji kwenye nafasi ya namba sita ni mwenye ushindani akimaanisha kutumia nguvu na mwenye uwezo wa kutibua kila aina ya shambulizi la kupitia katikati na pia kuanzisha mashambulizi kwa viungo na mawinga.
Alisema endapo atafanikiwa kumpata mchezaji mwenye sifa hizo anaamini Yanga, itafanya vizuri na kufika mbali kwenye michuano ya kimataifa mwakani kwa sababu atakuwa amelimaliza tatizo ambalo limechangia kwa kiasi kikubwa mwaka huu kufanya vibaya.
Pluijm, alisema bado hajampata mbadala wa Salum Telela ambaye atakuwa maalumu kwa ajili ya kusaidiana na Thabani Kamusoko ingawa amekuwa akimjaribu Mbuyu Twite lakini ameshindwa kutimiza majukumu yake ipasavyo na hiyo inatokana na kukosa nguvu na kupambana na vijana wenye umri mdogo kushinda yeye.
No comments:
Post a Comment