TIMU ya Azam FC inatarajiwa kuondoka leo kwenda Zanzibar kwa ajili ya kambi ya maandalizi ya msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaoanza mwezi ujao.
Azam FC itacheza na Yanga Agosti 17 katika mchezo wa Ngao ya Jamii, mahsusi kwa ajili ya uzinduzi wa msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara unaoanza Agosti 20.
Msemaji wa Azam FC Jaffar Idd alisema timu hiyo itaondoka na wachezaji wote wakiwemo na wale kutoka nje wanaojaribiwa wakitaka kusajiliwa.
Akizungumza na gazeti hili jana Idd alisema bado kocha wao, Zeben Hernandez anahitaji kuwatazama zaidi wachezaji walioko ili kufanya maamuzi sahihi ya nani atabaki kuendelea nao.
Alisema mchezaji ambaye hatakuwepo katika msafara huo ni kipa kutoka Hispania, Juan Gonzalez aliyeshindwa majaribio lakini wengine wote watakwenda. Hadi sasa Azam ina wachezaji wageni kutoka mataifa mbalimbali wanaofanya majaribio wakitaka kuichezea timu hiyo.
Wachezaji walioko ni Bruce Kangwa(Zimbabwe), Fuadi Ndayisenga (Burundi), beki Mohamed Chikoto(Niger), mastraika Ibrahima Fofana (Ivory Coast), Mossi Issa (Niger) na kipa wa Ivory Coast Daniel Yeboah.
Alisema ikiwa huko itacheza mechi mbalimbali za kirafiki kwa ajili ya kujipima nguvu. Katika maandalizi ya awali Chamazi, timu hiyo ilicheza mechi tatu za kirafiki dhidi ya Friend Rangers na kuibuka na ushindi wa mabao 2-1, dhidi ya Ashanti United na kushinda mabao 2-0 dhidi ya Kinondoni FC na kushinda 5-0.
No comments:
Post a Comment