Latest News

Mayanja aipa pole Yanga


KOCHA msaidizi wa Simba, Jackson Mayanja amewapa pole wapinzani wao Yanga kutokana na matokeo mabaya wanayoyapata kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, hatua ya makundi na kuwataka wasikate tamaa warudi kujipanga upya kwa ajili ya mwakani.
Yanga juzi ilikubali kipigo cha mabao 3-1 dhidi ya Medeama SC ya Ghana na kupoteza matumaini ya mabingwa hao wa Tanzania kucheza nusu fainali ya michuano hiyo baada ya kuwa na pointi moja katika michezo minne waliyocheza.
Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu jana, Mayanja alisema kinachowashinda Yanga ni kushindwa kutofautisha mashindano ya Kombe la Shirikisho yana utofauti mkubwa na yale ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara, ndiyo maana wamejikuta wakishindwa kufanya vizuri katika mechi zao nne walizocheza.
Kocha huyo alisema matokeo waliyoyapata Yanga kwenye michuano hiyo inapaswa yachukuliwe kama somo kwa kukirekebisha kikosi chao ili mwakani waweze kufanya vizuri kwa sababu bado watashiriki tena michuano hiyo kutokana na ubingwa walioutwaa msimu uliopita.
Alisema ugumu uliopo kwenye mashindano hayo alijua wazi kama Yanga wangekuwa washiriki kutokana na udhaifu wa kikosi walichokuwa nacho ambacho ushindani wake upo kwenye ligi ya ndani pekee na siyo kwenye michuano hiyo mikubwa Afrika.
Mayanja alisema Yanga wasitafute mchawi kwa sababu matokeo wanayoyapata hivi sasa walistahili kulingana na ubora wa timu waliyokuwa nayo na kuwatahadharisha wasipoangalia hali hiyo inaweza kuendelea kuwakuta hadi kwenye msimu mpya wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara inayotarajia kuanza Agosti 20.

No comments:

Post a Comment

PERUZI24HOURS Designed by Templateism.com Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.