KOCHA Mkuu wa timu ya soka ya taifa, Taifa Stars, Charles Mkwasa ameahirisha kambi ya timu hiyo iliyokuwa ianze Dar es Salaam kesho.
Taarifa kutoka kwa Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Alfred Lucas kwa waandishi wa habari jana ilisema kocha Mkwasa ameamua kuahirisha kambi hiyo baada ya kupata maombi mengi kutoka kwa timu zinazoshiriki Ligi Kuu.
Taarifa hiyo ilisema kutokana na hilo, Mkwasa atakuwa akifuatilia mwenendo wa nyota 24 aliowaita kwenye michezo mbalimbali ya kirafiki ya klabu hizo inayofanyika kwa ajili ya maandalizi ya kuanza msimu mpya.
Taifa Stars inatarajiwa kucheza Lagos, Nigeria Septemba 2 mwaka huu katika mechi ya makundi kuwaniakufuzu michuano ya Kombe la Mataifa Afrika itakayofanyika Gabon mwakani. Hata hivyo mechi hiyo ni kama kukamilisha ratiba kwani Stars haina uwezo wa kufuzu kwenye kundi lake baada ya Chad kujitoa na hivyo kubaki timu tatu.
Kundi hilo lilikuwa na timu za Tanzania, Chad, Nigeria na Misri ambayo ndiyo iliyofuzu michuano hiyo.
Kikosi cha Stars Makipa: Deogratius Munishi, Aishi Manula na Benny Kakolanya. Mabeki: Kelvin Yondani, Aggrey Morris, Oscar Joshua, Mohamed Husein ‘Zimbwe Jr’, Juma Abdul na Erasto Nyoni. Viungo: Himid Mao, Mohamed Ibrahim, Shiza Kichuya, Jonas Mkude, Ibrahim Jeba, Mwinyi Kazimoto, Farid Mussa, Juma Mahadhi na Hassan Kabunda.
Washambuliaji: Simon Msuva, Joseph Mahundi, Jamal Mnyate, Ibrahim Ajib, John Bocco na Jeremia Juma.
No comments:
Post a Comment