Latest News

Kikosi cha Simba hadharani wiki ijayo



KOCHA Mkuu wa timu ya soka ya Simba, Mcameroon Joseph Omog amesema kikosi kamili cha wachezaji kitakachoingia kwenye ushindani wa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa mwaka 2016/2017 kitawekwa hadharani wiki ijayo.
Omog alisema hayo alipozungumza na gazeti hili juzi kwenye uwanja wa Chuo cha Biblia cha Highland cha Kanisa la Baptist mjini hapa baada ya mechi ya kirafiki kati ya timu yake na Polisi inayoshiriki daraja la kwanza. Simba ilishinda mabao 6-0 katika mechi hiyo.
Alisema kikosi cha wachezaji atakachokiunda mwanzoni mwa wiki ijayo anaamini kitakuwa cha kuleta ushindi katika michuano ya Ligi Kuu. Ligi Kuu imepangwa kuanza kutimua vumbi Agosti 20 mwaka huu ambapo Simba itaanzia nyumbani dhidi ya Ndanda kwenye uwanja wa Taifa Dar es Salaam.
Omog alisema kuifunga timu ya Polisi Morogoro kwa bao 6-0 kwenye mchezo wa kirafiki haimaanishi kuwa timu imeiva na kuwa na kikosi imara kwa kuwa bado anahitaji muda zaidi wa kuwapatia wachezaji wake mafunzo na mbinu za kisasa za uchezaji wenye kuleta ushindi kwenye michuano hiyo.
Alisema alifurahi kuona tangu kuanza kwa mazoezi kwenye kambi hiyo wachezaji wamebadilika tofauti na mwanzo alipoanza kuwafundisha walipokuwa wametokea katika mapumziko.
Omog alisema kuwa licha ya mafunzo na mazoezi yanayotolewa kwa wachezaji hao bado inahitajika michezo mingine mitatu ama zaidi ya kirafiki kabla ya kuanza ligi.
Pamoja na hayo, Omog alimpongeza Kocha msaidizi wa timu hiyo Jackson Mayanja kwa kumpatia ushirikiano mkubwa katika programu za mazoezi kitendo kinachowezesha kuijenga upya timu ya Simba iweze kutwaa ubingwa msimu wa ligi.

No comments:

Post a Comment

PERUZI24HOURS Designed by Templateism.com Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.