Latest News

Maamuzi magumu Simba


KWA maamuzi yoyote yatakayoamuliwa leo kwenye Mkutano Mkuu wa Wanachama wa Simba juu ya kuuza hisa za klabu hiyo kwa mfanyabiashara bilionea Mohamed Dewji (Mo) itakuwa ni kufanya maamuzi magumu.
Mo aliyewahi kuwa mfadhili wa Simba alisema juzi kuwa yupo tayari kutumia Sh bilioni 5.5 kuendesha klabu hiyo kwa msimu kama atauziwa hisa asilimia 51 kwa Sh bilioni 20 kuimiliki.
Mo ni mpenzi na mwanachama wa Simba SC, ambaye kati ya 1999 na 2005 alikuwa mdhamini Mkuu wa klabu na akazishawishi pia Simba Cement na NBC kuwekeza katika klabu hiyo hadi ikafuzu hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2003 ikiitoa Zamalek ya Misri.
Mo pia amewahi kuwa mdhamini wa Singida United na mmiliki wa African Lyon kwa muda, kabla ya kuiuza kwa mfanyabiashara Rahim ‘Zamunda’ Kangenzi.
Tangu mwishoni mwa mwaka jana kulikuwa na tetesi kuwa mfanyabiashara huyo anayeshika nafasi ya 24 kwa utajiri duniani anataka kuinunua Simba, ila ikadaiwa kuwa tatizo lilikuwa kwa uongozi na baadhi ya wanachama ambao hawakuwa tayari kwa hilo.
Hivyo hali ya kukubali suala hilo kwa haraka katika mkutano wa leo utakaofanyika bwalo la Polisi la Oysterbay itakuwa ni kufanya maamuzi magumu kwa wale walioonekana kupinga suala hilo tangu mwanzo na pia mkutano huo ukikataa ofa hiyo ya Mo pia watakuwa wamefanya maamuzi magumu kukataa kitita kama hicho cha fedha hasa katika wakati huu ambao Simba ipo kwenye hali mbaya.
Awali Rais wa Simba, Evans Aveva alizungumza na gazeti hili na kuliambia kwamba kama Mo anataka kuinunua klabu apeleke hoja rasmi na si kuzungumza kwenye vyombo vya habari lakini pia suala hilo ni la kikatiba zaidi ni lazima taratibu zifuatwe na katiba ibadilishwe kwa idhini ya Mkutano Mkuu ili kuruhusu hilo lifanyike.
Mo akizungumza na vyombo vya habari juzi alisema anataka kubadilisha mfumo katika klabu hiyo, kama tu mkutano huo utaridhia lengo likiwa ni kuiokoa timu hiyo.
Alisema akiuziwa asilimia 51 ya hisa na kuwa mmiliki wa Simba atawaweze sha wanachama wa muda mrefu kupewa hisa bure ambazo wataamua wenyewe kuuza au kununua zaidi.
Alisema lengo lake ni kuifanya Simba itwae ubingwa wa Afrika kwa kushindana na timu kama TP Mazembe ya DR Congo zinazotumia bajeti ya Sh bilioni 20 kwa mwaka.
Wakati Simba ikitarajiwa kufanya mkutano huo na kutoa maamuzi juu ya kile anachopendekeza, alisema atakuwa Singida kwa mapumziko akisubiri jibu na kwamba iwapo watakubali au kutokubaliana hatakuwa na shida atakubaliana na maamuzi yao.
Alisema jambo la msingi ni Simba kubadili katiba yao ili kusaini mkataba na baada ya hapo wataanza utaratibu ambao unaweza kuchukua kuanzia miezi sita hadi mwaka.
Mo alisema kwa kuwa Simba ina majengo pacha mawili Mtaa wa Msimbazi, Kariakoo na kiwanja Bunju, atatumia Sh bilioni 5 kujenga uwanja wa kisasa ndani ya miaka mitatu.
Mbali na suala hilo la Mo, mkutano wa Simba leo pia utafahamishwa vizuri juu ya suala la fedha za Emmanuel Okwi Sh milioni 600 zilizolipwa na Etoile du Sahel ya Tunisia ilipomnunua takribani miaka minne iliyopita.
Mkutano huo pia utajadili ushiriki wa timu hiyo katika Ligi Kuu msimu uliopita ambapo ilimaliza ya tatu. Lakini pia ikikosa nafasi ya uwakilishi wa kimataifa kwa miaka minne mfululizo.

No comments:

Post a Comment

PERUZI24HOURS Designed by Templateism.com Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.