Latest News

Malinzi awafunda vijana wa ARS


RAIS wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Jamal Malinzi amewataka vijana kujituma ili kutimiza ndoto zao. Malinzi aliyasema hayo kwenye ufunguzi wa michuano ya kusaka vipaji vya soka kwa vijana chini ya umri wa miaka 17 ya Airtel Rising Stars (ARS) ngazi ya mkoa Dar es Salaam jana.
Aidha, Malinzi pia aliziomba klabu zinazoshiriki Ligi Kuu pamoja na Ligi Daraja ya Kwanza kutumia fursa ya Airtel Rising Stars kwa ajili ya manufaa yao.
“Michuano hii inatoa nafasi nzuri kwa klabu zetu kuja na kutambua vipaji vinavyoibukia na kuwasajili kwenye timu zao,” alisema.
Alisema michuano hiyo ni sehemu bora ya kutambua vipaji kwani Airtel Rising Stars inatoa fursa kwa wavulana na wasichana wanaoshiriki michuano kujitambua kimaisha.
Akizungumza na wachezaji kutoka mikoa ya kisoka Ilala, Kinondoni na Temeke Malinzi alisema wachezaji kufanya vizuri kwenye michuano hiyo ni kujitengenezea nafasi ya ajira.
Aliwakumbusha jinsi soka lilivyobadilisha maisha ya mchezaji Mbwana Samatta anayecheza KRC Genk ya Ubelgiji na Thomas Ulimwengu wa TP Mazembe ya DR Congo huku akisisitiza kwamba soka inatoa ajira kwa mamilioni ya wachezaji duniani kote.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Airtel Tanzania, Sunil Colaso aliwashukuru wadau wa soka kwa kusaidia na kushiriki kwao kwenye michuano ya Airtel Rising Stars kwa miaka mitano na kuwaomba makocha kuwachagua wachezaji wenye vipaji kwa ajili ya kuandaa timu ya kushiriki michuano ya taifa.
“Tunajivunia uhusiano wetu mzuri na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na Afrika kwa ujumla na tunayo furaha kuwa klabu na Timu za Taifa zinafaidika na matunda ya Airtel Rising Stars,” alisema Colaso.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Ufundi wa TFF Salum Madadi aliwapongeza Airtel kwa programu hiyo na kusema imesaidia kutafuta na kukuza vipaji vya soka nchini.
Michuano ya Airtel Rising Stars ngazi ya mkoa ikishirikisha Ilala, Temeke, Kinondoni, Mbeya, Morogoro, Mwanza, Lindi, Zanzibar na Arusha inatarajiwa kumalizika Septemba mwaka huu.

No comments:

Post a Comment

PERUZI24HOURS Designed by Templateism.com Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.