WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, amepiga marufuku vikao visivyo na tija vinavyofanywa na Mamlaka ya Bandari ya Tanzania (TPA) ambavyo hutumia zaidi ya Sh milioni 200.
Mbarawa alisema katika vikao hivyo, wajumbe hulipwa Sh 200,000 kila mmoja kwa kuhudhuria chini ya saa mbili na kueleza malipo hayo yanachangia wahusika kuishi kwa anasa iliyopindukia wakati fedha hizo zingeweza kuendeleza bandari ndogo zilizopo kwenye Ziwa Tanganyika katika mikoa ya Rukwa, Katavi na Kigoma.
Alimwagiza Mtendaji Mkuu wa TPA, Deusdedit Kakoko, kuona uwezekano wa kuvipunguza vikao hivyo sita na kubakiwa na vya kisheria pekee ikiwa ni jitihada ya kubana matumizi yasiyo ya lazima.
Aidha, aliwataka wajumbe kuhudhuria vikao vyenye tija siku nzima badala ya saa mbili huku wakilipwa kiasi kikubwa cha posho. Alivitaja vikao hivyo kuwa ni vya Baraza la Wafanykazi (Dowuta), bajeti na vya majadiliano ya bajeti.
“Mtendaji Mkuu wa TPA aone uwezekano wa kufanya “video conferences ‘ ni vikao ambavyo vinaweza kuwaunganisha wajumbe katika bandari za Mtwara, Kigoma, Tanga na Dar es Salaam kwa wakati mmoja hivyo kupunguza gharama zisizo za lazima," alisisitiza.
Profesa Makame alitoa maagizo hayo alipotembelea bandari ndogo ya Kasanga iliyopo katika Ziwa Tanganyika, wilayani Kalambo, ambako alistushwa na mfumo mbaya wa ukusanyaji wa mapato na utunzaji wa hesabu kwenye bandari hiyo.
Pia alisema taarifa ya utendaji wa bandari ndogo ya Kasanga, iliyosomwa na Meneja wa bandari hiyo, Selemani Kalugendo, haikuonesha malengo wala mapato ya bandari hiyo iliyoingiza katika kipindi cha miezi sita iliyopita.
No comments:
Post a Comment