MAHAKAMA ya Tanzania mkoani Iringa imezindua mpango utakaowawezesha wananchi katika mkoa huo kutumia simuza mkononi kutuma bure taarifa za watumishi wa Mahakama wanaokiuka maadili ya kazi, ikiwemo kujihusisha na vitendo vya rushwa.
Mkurugenzi Msaidizi wa Masuala ya Utawala wa Mahakama, Wanyenda Kutta, amesema mpango huo unaolenga kurejesha imani ya chombo hicho kwa jamii ni sehemu ya utekelezaji wa mikakati ya kuboresha mfumo wa uendeshaji wa Mahakama.
Aliyasema hayo jana wakati akimkabidhi Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza, simu nne kwa ajili ya matumizi ya Mkuu wa Mkoa na Wakuu wa Wilaya za Iringa, Kilolo na Mufindi wanaounda kamati za maadili.
Viongozi hao pia walikabidhiwa mabango yenye taarifa na namba za simu, zitakazotumiwa na wananchi wenye malalamiko kutuma taarifa hizo.
Alikabidhi simu na mabango hayo siku moja baada ya watumishi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Iringa kushiriki warsha ya siku moja iliyowapa mrejesho kuhusu Mpango wa Maboresho ya Kiutawala na Kiutendaji, yanayoendelea kufanywa na Mahakama ya Tanzania.
Kutta alisema mabango hayo yatabandikwa katika ofisi za serikali za ngazi zote, taasisi za umma na binafsi na sehemu zinazotoa huduma mbalimbali kwa jamii kama hospitali, vituo vya mabasi, teksi na bodaboda, viwanja vya michezo, shuleni, taasisi za dini, ofisi za vyama vya siasa na sokoni.
“Katika juhudi za kupambana na rushwa mahakama imeingia katika matumizi Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), ili kwa kushirikiana na wadau wake ipate mafanikio ya haraka. Mwito wetu kwenu ni kutoa taarifa za kweli ili mamlaka ziweze kuchukua hatua zinazostahili kwa mtumishi alitakayebainika amekiuka maadili,” alisema Kutta.
Alisema kwa kupitia namba zilizoko katika mabango hayo, taarifa za wananchi zitaifikia mara moja Mahakama ya Tanzania, Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru) na kamati za maadili na hivyo kufanyiwa kazi kwa haraka.
Akizungumzia mlundikano wa kesi katika Mahakama Kuu, Kanda ya Iringa, Naibu Msajili wa Mahakama hiyo, Ruth Masam alisema “Mwaka jana Mahakama ilikuwa na kesi za muda mrefu 48 lakini ongezeko la majaji, kutoka mmoja hadi watatu imewezesha kesi hizo kubaki tatu tu hadi sasa.”
No comments:
Post a Comment