WATU watatu wamekufa na wengine 30 kujeruhiwa baada ya gari walilokuwa wakisafiria kutoka msibani kugongana na lori linalotengeneza barabara ya Kondoa-Manyara katika eneo la Humai wilayani Kondoa Mkoa wa Dodoma.
Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana kutoka eneo la ajali, watu hao walikuwa wakitokea kwenye msiba wa ndugu yao aliyekuwa akiishi Palanda wilayani Chemba.
Taarifa zinasema ajali hiyo ilihusisha gari dogo la abiria aina ya Toyota Coaster namba T567 BAH lililokuwa likiendeshwa na Eliab Juma lililongana na lori aina ya Isuzu lenye namba za usajili T269 AZL, mali ya Kampuni ya CRG ya Wachina inayojenga barabara hiyo.
Dereva wa Isuzu alitambuliwa kwa jina moja la Alfa. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Lazaro Mambosasa, alisema ajali hiyo ilitokea saa 1:30 usiku wa kuamkia jana katika eneo hilo.
Amewataja waliokufa ni Hamida Juma (35), Abubakar Athuman (54) na Samira Amir (32), wakazi wa Mabogini, Moshi. Alisema dereva wa Isuzu anayedaiwa kusababisha ajali hiyo amekimbia na juhudi za kumtafuta zinaendelea.
Shuhuda wa ajali hiyo, Isihaka Kidundulu alisema chanzo cha ajali hiyo ni gari la Wachina kutokuwa na taa, hivyo kuwapa wakati mgumu waliokuwa katika basi.
No comments:
Post a Comment