KOCHA Mkuu wa Mwadui FC, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ amesema anatambia ubora wa kikosi alichokuwa nacho na kusema safari hii ana uhakika wa kubeba taji moja kati ya mawili ambayo ni lile la Ligi Kuu ya Tanzania Bara na la Kombe la FA, linaloandaliwa na Shirikisho la soka Tanzania (TFF).
Mwadui FC imesajili wachezaji wengi chipukizi kwa ajili ya msimu ujao na hiyo imetokana na kocha huyo kuwatema wachezaji wengi wakongwe ambao walimaliza mikataba yao mwishoni mwa msimu uliopita.
Akizungumza na gazeti hili jana Julio alisema amepania kuiona timu hiyo ikiweka rekodi kwa kubeba moja ya taji kati ya hayo mawili na kuliwakilisha taifa katika michuano ya kimataifa mwaka 2018.
“Nina imani na hilo kwa sababu nimefanya mabadiliko makubwa kwenye kikosi changu kwa kuleta damu changa ambazo naamini zitafanya kazi niliyowatuma kwa asilimia 100 na mwisho wasiku tutasherehekea kwa kile tulichokikusudia,” alisema Julio.
Kocha huyo mwenye maneno mengi alisema sababu ya kushindwa kuendelea na baadhi ya wachezaji wakongwe kwenye kikosi chake ni kushindwa kuendana na kasi ya mchezo kwenye ligi hiyo ambayo timu nyingi zinaundwa na wachezaji chipukizi.
Huu utakuwa msimu wa pili kwa Mwadui FC, kushiriki ligi ya Tanzania Bara baada ya msimu wake wa kwanza kumaliza nafasi ya sita kwenye msimamo wa ligi hiyo huku ikitolewa na Azam FC kwa mikwaju ya penalti katika hatua ya nusu fainali.
No comments:
Post a Comment