WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa amesema atafuatilia ili kubaini mazingira yaliyosababisha Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA) kutoa Sh milioni 20 kwa Taasisi ya Elimu ya Genesis wakati ikiwa haina sifa.
Waziri huyo amesema pia atachunguza ili kujiridhisha madai kuwa hatua hiyo, ilitokana na mgongano wa kimaslahi kutokana na mmoja wa wajumbe wa Bodi ya Taasisi ya Elimu ya Genesis, Dk Norman Sigalla ( Mbunge wa Makete CCM) kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu.
Hatua hiyo imekuja siku chache baada ya TAA kutoa fedha hizo kwa taasisi hiyo ya Genesis ya jijini Dar es Salaam na baadaye uongozi wa mamlaka hiyo kuamuru uongozi wa Genesis, kurejesha fedha hizo kwa maelezo ya kutokuwa na sifa.
Akizungumza na gazeti hili jana, Profesa Mbarawa alisema atafuatilia kwa kina suala hilo na kujiridhisha mazingira yake. Katika maelezo yake, TAA walisema hatua ya kuagiza fedha hizo kurejeshwa, inatokana na kubainika kuwa Taasisi ya Genesis haitambuliwi na Baraza la Taifa la Elimu na Ufundi (NACTE).
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili ulibaini kuwa Taasisi ya Genesis iliomba kwa TAA msaada wa Sh milioni 30 kwa ajili ya kusaidia ujenzi wa mabweni katika eneo la Isimani mkoani Iringa kupitia barua yenye kumbukumbu namba GISS/ TAA/002/016.
Hata hivyo taasisi hiyo ikiwa tayari imepewa Sh milioni 20, TAA waliandika barua yenye kumbukumbu namba DB.231/236/01F/79 ya Julai 14, mwaka huu iliyosainiwa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wake, George Sambali ikiagiza fedha hizo kurejeshwa.
Sambali alibainisha kuwa baada ya kupokea maombi kupitia Kitengo cha Kusaidia Huduma za Jamii (CSR), TAA iliamua kutoa fedha hizo kupitia Akaunti ya Genesis yenye namba 01J1042893500 iliyopo Benki ya CRDB tawi la PPF Tower jijini Dar es Salaam.
Kaimu Mkurugenzi huyo alisema kupitia barua hiyo kuwa TAA ilibaini baadaye kuwa ilikuwa imetoa fedha hizo bila kufahamu kuwa taasisi hiyo ya elimu, ilikuwa haitambuliwi na NACTE, jambo ambalo liliipotezea sifa ya kupewa fedha hizo.
Kwa upande wake, Dk Sigalla pamoja na kukanusha kuwepo kwa shinikizo lake ili kuisaidia taasisi hiyo ya Genesis ambayo yeye ni mjumbe wa Bodi, alieleza kushangazwa na madai ya TAA kuagiza fedha hizo zirejeshwe kwa madai ya taasisi hiyo kutokuwa na sifa, jambo ambalo si sahihi.
“Kwanza nikufahamishe tu kuwa fedha hizo zilirudishwa tangu Julai 18, mwaka huu. Hata hivyo si kweli kwamba Taasisi ya Genesis haina sifa, hayo ni madai ya ajabu sana. Hii ni taasisi iliyosajiliwa na kuendesha shughuli zake kwa mujibu wa sheria za nchi,” alisema.
No comments:
Post a Comment