Latest News

Simba ndio basi tena


SIMBA ya Dar es Salaam imepata pigo la aina yake baada ya pointi tatu ilizopewa mezani kurejeshwa kwa Kagera Sugar. Mbali na kupokwa pointi tatu, awali Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Soka Tanzania, TFF, ilimfungia mwaka mmoja msemaji wa timu hiyo, Haji Manara na kumpiga faini ya Sh milioni 9.
Akizungumza na waandishi wa habari jana Katibu Mkuu wa TFF, Selestine Mwesigwa alisema kuwa katika kikao chake Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji imebatilisha uamuzi uliochukuliwa na Kamati ya Saa 72, kutokana na kuwa upungufu mwingi.
Kamati ya Saa 72 iliwapa Simba pointi tatu baada ya timu hiyo kukata rufaa ikidai kuwa Kagera Sugar ilimchezesha mchezaji Mohamed Fakhi aliyekuwa na kadi tatu za njano. Alisema, kamati hiyo haikukidhi matakwa yaliyotakiwa ili kusikilizwa kwa hoja za Simba ambapo alitaja masharti hayo kuwa ni kushindwa kulipa ada ya malalamiko ambayo ni Sh 500,000.
Simba haikuwakilisha malalamiko yake kwa wakati husika ambao unatakiwa kuzingatiwa pamoja na kushirikishwa kwa wajumbe wasiokuwa na sifa kwenye mkutano huo. “Simba ililalamikia suala lake hilo bila ya kuzingatia taratibu kwa kuwa ilishindwa kuzingatia kanuni sahihi kwa kuwa kanuni ya 20 katika vifungu tofauti kifungu cha kwanza kimeweka wazi kuwa klabu inatakiwa kuwasilisha malalamiko yao ndani ya saa 72 huku kile cha pili kikiweka wazi kuwa ada ni lazima ilipwe yote kwa wakati,” alisema Mwesigwa.
Aliongeza: “Hiki kinachowakuta Simba leo (jana) ni sawa na kile kilichoikumba timu ya Polisi ambayo nayo iliilalamikia Simba, lakini haikulipa ada ya kusikilizwa kwa shauri lao”. Pia alisema kuwa kamati hiyo imeitaka bodi ya Ligi kuwafikisha katika kamati ya maadili maofisa wake wawili kwa kosa kimaadili ambapo Katibu huyo hakutaja majina ya maofisa.
“Suala la maofisa hawa wa Bodi ya Ligi kwa uzembe au kushindwa kuzingatia maadili ya kazi watatakiwa nao kuwajibishwa na kuhusu suala hilo aulizwe zaidi Ofisa Mtendaji Mkuu wa Bodi hiyo,” alisema Mwesigwa. Simba sasa ina pointi 59 baada ya kuchukuliwa pointi hizo wakati Yanga ikiendelea kubaki katika nafasi ya pili ikiwa na pointi 56 lakini ina mechi mbili mkononi.

No comments:

Post a Comment

PERUZI24HOURS Designed by Templateism.com Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.